Wakurugenzi wapya 13 wa halmashauri wameapa
kulinda maadili na kukabidhiwa majukumu ya kufuatilia maagizo ya Rais,
Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, kwenye maeneo yao na kutoa mrejesho wa
hatua za utekelezaji wake. Kiapo hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki
aliyewataka kutilia mkazo ufuatiliaji wa maagizo na kupambana na tatizo
la watumishi hewa ambao idadi yao imefikia 17,102 waliogundulika katika
kipindi cha kuanzia Machi mpaka sasa.
Wakurugenzi hao walioteuliwa hivi
karibuni na Rais, John Magufuli waliapishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George
Simbachawene katika ukumbi wa Tamisemi mjini Dodoma.
Akizungumza mara
baada ya kiapo hicho, waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi hao
kutekeleza matamko yote yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu
serikalini, kwa kutoa mrejesho wa utekelezaji wake.
Kairuki aliwataka
kufanya kazi kwa bidii ili wawatumikie wananchi wanaowaongoza.
Alisema
katika ziara nyingi alizozifanya, amekuta wakurugenzi hawafuatilii
matamko yanayotolewa na viongozi wa ngazi za juu serikalini katika
maeneo yao.
“Hata kwa wale ambao wanayafuatilia huwa hawatoi mrejesho wa
hatua zilizofikiwa katika kutekeleza matamko hayo, hivyo ninawaomba
mkayatekeleze maagizo na kurudisha mrejesho kwa kiwango kinachotakiwa,”
alisema Kairuki.
Pia, aliwataka wakurugenzi hao kwenda kusimamia fedha
za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali hadi senti ya mwisho,
ili kuhakikisha inatekelezwa kwa asilimia 100.
Alisema kuna baadhi ya
miradi ya maendeleo, inatekelezwa kwa fedha za Serikali na wakati huo
huo inatumia fedha za wafadhili.
Waziri Kairuki aliwataka wakurugenzi
hao kuhakikisha kuwa miradi yote inayotumia fedha za Serikali
inasimamiwa ipasavyo.
“Utakuta mradi mmoja unafadhiliwa na pia
unatumia fedha za Serikali, kwa hiyo wafadhili wakija kukagua
wanaonyeshwa jengo likiwa limekamilika na Serikali nayo ikija kukagua
inaonyeshwa jengo hilohilo. Nataka mkasimamie fedha zote za Serikali
kwenye mamlaka zenu,” alisema Kairuki.
Alisema kuna baadhi ya maeneo ambako fedha
za Tasaf (mpango wa kunusuru kaya maskini), zimetumika kujengea maabara
na kununulia madawati kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Pia, aliwataka
kuhakikisha kuwa hatua kali za kinidhamu zinachukuliwa kwa wakati kwa
watumishi waliosimamishwa kazi katika kipindi cha miezi sita na si zaidi
ya hapo.
Alisema mtumishi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo
kufukuzwa au kusimamishwa kazi, mchakato wake wote ufanyike ndani ya
miezi sita.
Aliwataka pia wakurugenzi hao kufuata maadili ya viongozi wa
umma, kwani wakikiuka watafikishwa kwenye baraza la maadili ya viongozi
wa umma ambalo kwa sasa limeongezewa meno.
Waziri Kairuki aliwataka
wakurugenzi hao kusimamia suala la rasilimali watu, kwani utafiti
ulionyesha kuwa asilimia 80 hadi 90 ya watumishi wa umma ni watoro.
Alisema katika baadhi ya maeneo kuna wakaguzi na waratibu wa elimu wa
kata, lakini hawatembelei shule zao kuona kama walimu wanahudhuria
shuleni au la.
Kadhalika, aliwataka wakurugenzi hao kuachana na tabia
ya kuwatumia viongozi wa Serikali walioko chini yao, kama vile watendaji
wa kata, vijiji na wenyeviti wa vijiji kuwalimia mashamba yao.
Alisema
watakaobainika kufanya vitendo hivyo, watachukuliwa hatua kali za
kinidhamu.
Waziri Simbachawene aliwataka wakurugenzi hao kwenda kuchapa
kazi bila kumwonea yeyote. Aliwaambia kuwa kukusanya mapato kiwe ni
kipaumbele chao cha kwanza, kwani kipimo cha mamlaka yoyote kujitegemea
ni uwezo wake wa kukusanya mapato.
Aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha
kuwa wanawatembelea watumishi wao wote ili kujua penye upungufu, idadi
yao na hata ikiwezekana kuwajua kwa majina yao.
Wakurugenzi walioapishwa
jana ni Godwin Kunambi (Dodoma) Elias Ntiruhungwa (Tarime), Mwantumu
Dau (Bukoba) na Frank Bahati (Ukerewe) Wengine ni Hudson Kamonga
(Mbulu), Mwailwa Pangani (Nsimbo), Godfrey Sanga (Mkalama), Yusufu
Semuguruka (Ulanga), Bakari Mohamed (Nachingwea), Juma Mnweke (Kibondo),
Butamo Ndalahwa (Moshi), Waziri Mourice (Karatu) na Fatma Latu
(Bagamoyo).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki
akiongea Wakurugenzi wapya mara baada ya kuapishwa jana mjini Dodoma.
Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene. Kushoto kwa Simbachawene
ni Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilimanjaro Bi. Butamo
Nuru Ndalahwa
No comments:
Post a Comment