WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameelezea
masikitiko yake juu ya kuharibika ndani ya muda mfupi kwa mitambo ya
kufua na kuzalisha umeme na kuongeza kuwa, jambo hilo linamkera mno.
Aidha, amesema ili kuiondolea mikoa ya Lindi na Mtwara tatizo la
kukatika mara kwa mara umeme, nguvu kubwa inaelekezwa katika kuhakikisha
mikoa hiyo inaingizwa katika Gridi ya Taifa. Profesa Muhongo aliyasema
hayo bungeni jana wakati akitoa majibu ya ufafanuzi katika swali la
nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF).
Ngombale alitaka kufahamu hatua ambazo serikali inachukua kukabiliana
na uharibifu wa mitambo inayoharibika ndani ya muda mfupi baada ya
kujengwa kwake. Katika swali la msingi, alitaka kufahamu kama serikali
inaweza kuwaambia wananchi kiini hasa cha kukatika kila siku kwa umeme
unaozalishwa kutokana na gesi ya Songosongo.
“Hapa tusidanganyane, ni ukweli usiopingika kuwa, mitambo ya Somanga
Fungu ina matatizo makubwa, licha ya kuwa ilijengwa kama miaka miwili
iliyopita,” alisema Profesa Muhongo na kupongeza kuwa mbali ya mitambo
hiyo, lakini pia mitambo ya Nyakato, Mwanza na ya Ubungo, Dar es Salaam
nayo imekuwa na shida, kwani ilianza kuharibika miaka miwili baada ya
kujengwa.
“Kwa nini iharibike baada ya miwili miwili? Tusidanganye….kuna
tatizo,” alihoji Profesa Muhongo na kuongeza kuwa ili kukabiliana na
adha ya umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara, serikali imeona suluhisho
ni kuiunganisha katika Gridi ya Taifa na kwamba kazi ya kujenga njia
mpya ya umeme wa kilovoti 132 ili iachane na umeme wa kilovoti 33 wa
sasa, inaendelea."
Alisema kama kila kitu kitakwenda sawa, kazi hiyo inatarajiwa
kukamilika Novemba mwaka huu na kwamba mradi huo utagharimu Sh bilioni
3.
No comments:
Post a Comment