*Asema safari imeiva, ataka wajipange kuhamia Dodoma
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema safari ya kuhamia Dodoma imeiva na
amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wajipange kisaikolojia.
Ametoa
kauli hiyo jana (Jumatano, Agosti 18, 2016) alipokutana na kuzungumza na
watumishi wa ofisi yake kutoka taasisi, idara na vitengo mbalimbali
waliopo Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu aliwataka watumishi hao watambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia
Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao
chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano
Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
“Tangu
wakati huo kumekuwa na juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuandaa
miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji
wa miundombinu hiyo,” alisema.
“Pia
tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai
23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena
Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo
hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.
“Napenda
kuwatoa hofu, mambo yanaenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva sasa.
Kikubwa ni kwamba tutakwenda kwa awamu kama ambavyo imepangwa,”
alisema.
“Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo. Tufanye kazi kwa bidii. Tuhakikishe kila kilichopangwa kinafanyika kwa ufanisi na kinafanikiwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment