Tuesday, August 2, 2016

WAKUU WA IDARA WILAYANI IKUNGI, MAAFISA TARAFA, WATENDAJI WA KATA, VIJIJI NA WENYEVITI WA VIJIJI WAFUNDWA





Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwasilisha mtazamo wa namna ambavyo anataka Wilayahiyo iwe




Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji





Afisa utumishi wa Wilaya ya Ikungi Evodius Buberwa akifafanua na kutofautisha majukumu ya watendaji wote ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji






Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza umuhimu wa kuchangia maabara kwa ajili ya kuwanusuru wanafunzi wanaotaka kusoma masomo ya sayansi lakini kikwaza inakuwa maabara

 





Kutoka Kushoto ni Mustafa Mtopo kaimu Afisa usalama wa Taifa Wilaya ya Ikungi, Fortunatus Ndalama Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Ikungi, Dijovson Ntangeki Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya ikungi Rustika Turuka, na Mkuu wa poiisi Wilaya ya Ikungi Milton Nkyalu wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji waliotoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo




Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya ikungi Rustika Turuka aliyesimama akizungumza na Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakati wa kikao hicho cha kazi



Afisa utumishi wa Wilaya ya Ikungi Ahmed Mussa akiwasilisha madawakati wa mafunzo hayo



Kaimu katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi Dijovson Ntangeki akielezea ratiba ilivyo ya mafunzo hayo


Na Mathias Canal, Singida

Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji 101 vilivyopo Wilayani Ikungi Mkoani Singida hii leo wamepatiwa mafunzo ya kutambua mipaka ya majukumu yao kiutendaji katika kikao cha kazi kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Ikungi.

Mafunzo hayo yameandaliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na kubainika kuwa asilimia kubwa ya watendaji hususani wenyeviti wa vijiji na vitongoji wamekuwa wakiingilia katika majukumu ya kiutendaji.

Akifungua mafunzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya masaa matano yaliyojikita zaidi kutoa ufafanuzi juu ya majukumu ya watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji, Mkuu wa Wilaya hiyo Miraji Jumanne Mtaturu amebainisha kuwa pamoja na mafunzo kwa ajili ya ufahamu wa majukumu ya watendaji hao lakini amesema kuwa Wilaya ya Ikungi ipo nyuma kielimu kutokana na shule kuwa mbali na maeneo ya watu, wanafunzi wa kike kuachishwa shule na kuolewa, baadhi ya viongozi na wataalamu kutotimiza wajibu wao na wakati mwingine uzembe wa baadhi ya watumishi wa serikali katika kutatua kadhia za wananchi.

Pamoja na hayo pia DC Mtaturu amesema kuwa kuna baaadhi ya maeneo kuna shule ambazo zina majengo mazuri na Hosteli kwa ajili ya wanafunzi lakini wazazi wanakataa kuwapeleka wanafunzi shuleni ikiwa ni pamoja na shule ya Sekondari Mkinya iliyopo Kata ya Dung’unyi, Shule ya Sekondari Mtunduru, Shule ya Sekondari Mwaru na Wembere , huku shule ya Sekondari Issuna ikiwa na Majengo na Hosteli nzuri lakini wanafunzi wanaosoma hapo ni wale wanaotoka Wilaya nyingine huku wenyeji wakiwa wamejichimbia ndani. 

Dc Mtaturu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Polisi kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua baadhi ya Watendaji wa Kata, Waratibu wa elimu wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji wanaoshirikiana na baadhi ya wazazi kuwaachisha wanafunzi shule ili wakaolewe ambapo amebaini kuwa katika Kata ya Mwaru na baadhi ya Kata zinazozunguka katika Kata hiyo viongozi wake kwa kushirikiana na Waratibu elimu Kata wamekuwa wakifanya biashara ya kuruhusu wanafunzi kuolewa kwa kupewa Ng’ombe.

Hata hivyo pia amewaagiza Watendaji wa Kata ya Makilawa na Iyumbu kumpatia taarifa ya kamati ya maendeleo ya Kata (WDC) ili kubaini mpango wa mikakati katika kujenga shule za Sekondari katika Kata hizo mbili ambazo zimesalia ilihali Kata 28 tayari zina shule za sekondari kati ya Kata 30 zilizopo katika Wilaya hiyo.

Katika shule 28 ni shule 3 tu zenye maabara, shule ya Sekondari ya Puma na Wembere ambao nao walijenga maabara baada ya kupata msaada kutoka Benki ya dunia Mwaka 2013, shule ya Sekondari Mkinya ina maabara 2 ambazo zilijengwa kwa msaada wa SADC mwaka 2009 hivyo kupelekea Wilaya nzima ya Ikungi kuwa na Maabara 4 pekee zilizojengwa kwa msaada wa wahisani ambapo hakuna hata maabara moja iliyojengwa na wananchi ikakamilika kutokana na zuio la kuchangia walilolipata wananchi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu.

Sawia na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya amewaagiza Watendaji wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji kuwaelimisha wananchi kukaa vikao na kupitisha maadhimio ya kuendelea kuchangisha michango ya ujenzi wa maabara kwa mujibu wa waraka wa Elimu namba 6 wa mwaka 2015 wa elimu msingi bila malipo.

Hata hivyo agizo limetolewa pia kwa Wazazi/Walezi pamoja na wanafunzi wenyewe kuchukuliwa hatua kali za kisheria kutokana na utoro wa wanafunzi shuleni jambo ambalo linapelekea kuwa na ufaulu duni wa wanafunzi Wilayani humo.

Dc Mtaturu pia amemuagiza Afisa Mtendaji wa Katana Afisa Mtendaji wa Tarafa kutumia siku 14 kuhakikisha madawati yanafika katika shule zenye uhaba wa madawati ili kuondokana na adha ambayo inaendelea kuwakumba wanafunzi shuleni ilihali madawati tayari yamepatikana.

Aidha ndani ya siku tano viongozi hao wameagizwa kuhakikisha kuwa Masoko pamoja na stendi zinaenda katika maeneo yaliyopangiwa ili ushuru upatikane kwa wakati na kwa kiasi kilichokusudiwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka amewashukuru Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa Vijiji kwa kujitokeza kwa wingi katika mafunzo hayo jambo ambalo limeonyesha kuwa wananchi hao wana imani na serikali ya awamu ya nne hivyo amewaomba kuachana na siasa na kufanya kazi kwa moyo na nguvu zaidi.

Amewataka viongozi wote wa ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na vitongoji kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na serikali kwa haraka na kwa ukamilifu.

Turuka amesema kuwa kila kiongozi anapaswa Kutatua kero za wananchi kwa kutenda haki, kutofanya kazi kwa mazoea, kutoa majawabu sahihi ya wananchi na kama hawafahamu wanapaswa kuuliza sehemu husika ili kutozungumza jambo wasilokuwa na uhakika nalo.

Kupitia kikao hicho kilichoitishwa na mkuu huyo wa Wilaya kilichokuwa na dhumuni la kufahamiana na kukumbushana majukumu na wajibu wa viongozi na kueleza mtazamo wa Ikungi mpya inavyotakiwa kuwa Afisa utumishi wa Wilaya sawia na Mkuu wa Polisi Wilaya wamepewa nafasi ya kuelezea majukumu na wajibu wa kila mmoja katika maeneo yao.

Kwa upande wao baadhi ya Watendaji wa Kata, Vijiji na wenyeviti wa vijiji 101 vilivyopo Wilayani humo wamesema kuwa mafunzo waliyoyapata watayatumia vyema kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi na kuwaelimisha zaidi ili kutambua mipaka yao na majukumu yao katika kuishauri serikali.

Aidha Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji wote ambao hawajahudhuria kikao hicho cha kazi wametakiwa kuandika barua za maelezo kwanini wameshindwa kuhudhuria na zimetakiwa kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi hadi kufikia tarehe 10 ya mwezi huu wa nane.

No comments:

Post a Comment