Tundu
Lissu, ambaye ni wakili wa Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya jana
alitumia muda wa saa mbili kupangua maombi ya wananchi wanne wanaopinga
matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi mteja wake.
Kesi
hiyo imeanza kusikilizwa tena baada ya Mahakama ya Rufaa kufuta uamuzi
wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali hoja za kupinga matokeo hayo, ambazo
ziliwasilishwa na wafuasi wanne wa aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo,
Steven Wasira (CCM).
Jaji
Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu, alitupilia mbali kesi hiyo baada ya
kukubali pingamizi la Lissu kuwa wafuasi hao hawakuwa na haki ya
kisheria kufungua kesi hiyo.
Wakazi
hao wa Bunda wanadai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kutokana na
kugubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanayemuunga mkono kunyimwa
fursa ya kuhakiki matokeo na pia kuongezeka kwa idadi ya vituo vya
kupigia kura.
Jana,
Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na wakili wa kujitegemea,
alitoa majibu ya utetezi mbele ya Jaji Lameck Mlacha kuanzia saa 4.10
asubuhi na kukamilisha saa 6.02 mchana wakati shauri hilo
lilipoahirishwa kwa muda hadi saa 8:00 mchana kutoa fursa kwa mawakili
wa upande wa wadai, Constantine Mutalemwa kujibu.
Lissu
alidai kuwa waleta maombi wameshindwa kutoa hoja mahususi kuonyesha
ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wanazodai ulikuwepo
katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Wakili
Lissu pia alidai kuwa walalamikaji ambao ni Magambo Masato, Matwiga
Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malegele, pia wameshindwa kuonyesha
madhara waliyopata kama wapigakura kuishawishi mahakama kutengua matokeo
yaliyompa ushindi Bulaya dhidi ya mwanasiasa huyo mkongwe.
“Waleta
maombi wanadai uchaguzi haukuwa huru na haki, idadi ya wapigakura
kutofautiana kwa kila kituo na uwepo wa vitendo vya rushwa, lakini
hawabainishi wazi nani mhusika wa mambo wanayoyalalamikia na madhara
waliyopata kwa nafasi yao ya wapigakura,” alisema wakili Lissu.
Alisema
vitendo vya rushwa katika uchaguzi ni kosa kubwa linaloweza kusababisha
kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi mzima, lakini walalamikaji wana
wajibu wa kumtaja mhusika wa vitendo hivyo ili kuipa mahakama fursa ya
kutafsiri vyema sheria na kutoa haki.
“Lakini
madai ya juujuu tena ya jumla kuwa aliyetoa rushwa ni wakala wa mteja
wangu, hayakubaliki mbele ya macho ya sheria kwa sababu mtu huyo
hajulikani na jukumu la kuthibitisha madai ni la mleta maombi na
uthibitisho huo haumo kwenye hati yao ya maombi,” alidai Lissu.
Aliomba
maombi hayo yafutwe kwa hoja kwamba wadai hawajataja vifungu vinavyoipa
mahakama haki na mamlaka ya kuyasikiliza na kuyaamua.
No comments:
Post a Comment