Friday, August 5, 2016

TRA yavuka lengo la ukusanyaji kodi mwezi Julai

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imevuka lengo la ukusanyaji wa kodi wa jumla ya kiasi cha shilingi trilioni 1 sawa na asilimia 95.6 tofauti na lengo lililokuwa limekusudiwa la kukusanya trilioni 1.1 kwa mwezi Julai 2016.

Kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 15.43 ukilinganisha na makusanyo ya awali ya mwaka 2015 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 914.

Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jjijini Dar es Salaam.

“Kwa mwezi Julai mwaka huu makusanyo yameongezeka kwa asilimia 15.43 ukilinganisha na kipindi cha mwezi Julai 2015 ambapo tulikusanya shilingi Bilioni 914” alisema Kayombo.

Aidha aliongeza kuwa mamlaka imeweka mikakati thabiti ya kuhakikisha kuwa inafikia au inavuka lengo la Serikali la kukusanya shilingi trilioni 15.1 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 huku mkakati mmoja wapo ukiwa ni kuhakikisha kuwa walipa kodi wapya wanasajiliwa zaidi.

Bw. Kayombo aliongeza kuwa mkakati mwingine ni kuhuisha taarifa za walipa kodi kwa kuhakikisha kwamba namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) zisizotumika zinafutwa katika mfumo wa TRA.

Pia amefafanua kuwa maandalizi ya kuhuisha taarifa za walipa kodi yapo katika hatua za mwisho ikiwemo upigaji picha,uchukuaji wa alama za vidole pamoja na vielelezo muhimu.

TRA inawakumbusha wananchi kuhakikisha wanakagua tiketi/risiti zao za manunuzi na kuangalia usahihi wa pesa walizolipa na uhalali wa risiti yenyewe.

No comments:

Post a Comment