WATU
wanaosadikiwa kuwa ni polisi mkoani Shinyanga wanadaiwa kuanzisha
vurugu baada ya kuagiza chipsi na kukataa kuzilipa, kisha kuanza
kuwapiga wauzaji na kuwabambikizia kesi.
Tukio
hilo linaelezwa kuwa lilitokea hivi karibuni katika eneo la Mshikamano,
kata ya Ngokolo, katika Manispaa ya Shinyanga majira ya usiku, wakati
askari hao wakidaiwa kwenda kwa muuza chipsi kwa ajili ya kununua.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii, Salumu Saidi ambaye ni muuza chipsi
aliyedai kufanyiwa vurugu, alisema askari hao walikuwa zaidi ya wanne,
lakini wawili ndio walioomba wakaangiwe chipsi.
“Wakati
naweka chipsi katika chombo cha kukaangia walianza kula kabla ya kuiva
na nilipotaka kuweka mayai waliniambia niongeze kwa madai kuwa ni ndogo
na ndipo nilipokataa kwa kuwa kipimo ni hicho, lakini walikataa kulipa,” Saidi alisema.
Alidai
kuwa baada ya mzozo kuibuka, mteja mmoja aliyekuwa ndani ya duka
lililopo karibu na biashara hiyo, aliwasili na kuulizia kuhusu malipo
huku akiwa amelewa na kuanzisha vurugu, lakini ghafla gari la Polisi
lilifika kwenye eneo hilo na kumbeba hadi kwenye kituo cha Polisi
alikofunguliwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia nguvu.
Kwa
upande wake, muathirika mwingine wa tukio hilo, Dotto Machunda ambaye
ni muuza matunda katika eneo hilo, alisema aliona vurugu katika maeneo
ya Darajani na baadaye kuona polisi katika kibanda chake ambao walianza
kumpiga na kisha kuondoka na kurejea kwenye eneo hilo baada ya muda
mfupi.
“Niliambiwa
nivue mkanda na kuwekwa ndani kuunganishwa kwenye makosa, lakini mpaka
leo hii sijapata matibabu, niliwaomba PF3 nikatibiwe walikataa wakati
nipo ndani na nilipotoka walininyima pia. Nilipokwenda hospitali ya mkoa
kutibiwa waliniambia kwa kuwa nimepigwa mpaka PF3, mpaka sasa sijapata
matibabu,” alisema Machunda.
Mwenyekiti
wa Mtaa lilipotokea tukio hilo, Victor Ochieng, alikiri kujua tatizo
hilo na kwamba alikwenda kwenye eneo la tukio kupata maelezo ya wananchi
wake kisha kufika Kituo cha Polisi kujua kinachoendelea.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa huu, Muliro Jumanne, alikiri kupokea taarifa lakini
alieleza kuwa alizozipata zilihusu askari wao kuvamiwa na wananchi.
Alisema
hata hivyo uchunguzi unaendelea kubaini wahusika wa tukio hilo ili
sheria ichukue mkondo wake, kwa sababu hakuna anayeruhusiwa kufanya
vurugu hata kama ni polisi.
No comments:
Post a Comment