NI ziara ya kwanza ya kiserikali ya Rais John Magufuli mkoani Mwanza tangu achaguliwe kuwa Rais.
Wakazi wa mkoa wa Mwanza wamejitokeza kwa wingi kumpokea wakiongozwa na viongozi wa serikali. Vikundi mbalimbali vya burudani vinatumbuiza. Kila eneo analopita (wilaya za mkoani Mwanza), anapata mapokezi ya aina yake. Akiwa jijini Mwanza, Rais ambaye aliongozana na mkewe, Janeth alipokelewa na maelfu ya wakazi waliosimama barabarani kabla ya kuhutubia jumla ya mikutano 11 akiwa njiani kuelekea Ikulu ndogo.
Akiwa katika Viwanja vya Furahisha, Magufuli alikiri kwamba, Mwanza imevunja rekodi kwa mapokezi makubwa na ya kishindo waliyompatia. Bila shaka mapokezi hayo na hasa anayopata mjini Mwanza, yanamkumbusha siku alipohitimisha kampeni za uchaguzi mkuu kabla ya kuibuka mshindi wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Vilevile ziara hiyo ya siku mbili imeleta faraja kwa makundi mbalimbali na wakati huo huo kuleta ‘simanzi’ kwa watu/taasisi waliojikuta wakimulikwa kutokana na kasoro mbalimbali zinazokwenda kinyume na msimamo wa Magufuli wa kuhudumia wanyonge.
Hali hiyo imejidhihirisha kutokana na hotuba zilizosheheni ushauri, makaripio, maonyo, hadhari, pongezi na hata maneno ya kuliwaza kwa makundi husika huku akisisitiza wananchi kufahamu msimamo wake wa kile anachohitaji katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni kuhudumia watu wanyonge. Falsafa yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ anaendelea kuieneza kwa kuwataka wananchi kufahamu kuwa ndiyo msimamo wake.
Anawataka wajenge tabia ya kufanya kazi kwa bidii wajikomboe kiuchumi na wawe na uhakika wa chakula. Anakemea watu wasiofanya kazi wakitarajia kuomba serikali iwapatie chakula.
“Serikali yangu haina chakula cha bure kwa mtu ambaye hafanyi kazi”, anasema. “Mtu unaamka asubuhi, unakwenda kucheza pool unawaacha baba na mama yako wakihangaika kulima, halafu useme serikali ikuletee chakula cha bure, hilo ndugu zangu haliwezekani. “Haiwezekani Tanzania ya leo yenye watu zaidi ya milioni hamsini badala ya kutengeneza barabara, kutafuta dawa za kujenga zahanati, kutoa elimu bure, itafute fedha za kusambaza umeme vijijini na badala yake itafute fedha za kuwapelekea chakula cha bure wananchi ambao hawafanyi kazi . Nasema Serikali ya Magufuli haitafanya hivyo,” anaweka wazi msimamo wake. “Nataka Watanzania wajue msimamo wa Serikali yangu ninayoiongoza,” anasema akisisitiza kuwa hata kijijini kwake Lubabangwe alikozaliwa, hawezi kupeleka chakula cha bure kwa watu ambao hawafanyi kazi.
Miongoni mwa viongozi ambao anaendelea kuwapa hadhari, ni pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya, akisisitiza kuwa hakuwateua kukaa ofisini. Anawataka wahamasishe wananchi kwenye maeneo yao washiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji wa chakula . Ziara hiyo inatoa faraja na matumaini makubwa kwa makundi mbalimbali hususani wakulima kutokana na Rais Magufuli kupiga marufuku halmashauri kuwatoza ushuru wanaosafirisha mazao yao kutoka shambani.
Badala yake, anawataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote na mabaraza ya madiwani kuhakikisha wanatoza ushuru kwa wafanyabiashara wakubwa wanaosafirisha mazao kwa magari makubwa. “ Madiwani mlichaguliwa na wananchi kama nilivyochaguliwa mimi, kama kuna by laws (sheria ndogo) ya kukusanya ushuru wa gunia mbili hadi tatu kwa wananchi masikini mkaifute sheria hiyo”, anasema.
Wakuu wa mikoa wanatwishwa mzigo kuhakikisha suala hilo wanalichukulia kwa umuhimu wa kipekee ili ushuru uwahusu wafanyabiashara wakubwa. Kumbukumbu za kampeni Lakini pia, ziara hiyo imerejesha kumbukumbu za kipindi cha kampeni ambazo Magufuli akiwa mgombea, alizihitimisha mjini Mwanza ambako aliacha ahadi mbalimbali juu ya Tanzania anayoitaka. Anawashukuru wakazi wa mkoa wa Mwanza kwa kumchagua kwa kura nyingi na hivyo kumwezesha kuwa Rais.
Anawakumbusha namna alivyowaahidi kutowaunganisha kwenye masuala ya maendeleo. “Nilifika hapa katika uwanja huu, nikiwa na wenzangu wengi, lakini mlinia mini na mkanichagua kuwa Rais wenu, nawashukuru sana, nasema sitawaangusha,” ni kauli aliyoitoa alipowahutubia wakazi wa wilaya ya Sengerema kwenye viwanja vya Mnadani. “Nataka niwaeleze deni limebaki kwetu, nyie mmemaliza kazi yenu deni ni ahadi nataka niwaahidi kama nilivyokuja kuwaomba kura sitawaangusha, nataka kutengeneza Tanzania mpya”, anasisitiza.
Miongoni mwa mambo ambayo anawahakikishia wakazi wa Sengerema, ni kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji . Pia anasema serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Sengerema- Kamanga kwa kiwango cha lami wakati upembuzi yakinifu ukiendelea. Habari njema nyingine ambayo wananchi wameipata kupitia ziara hiyo, ni juu ya taarifa kwamba, maeneo ya Usagara wilayani Misungwi na Buhongwa wilayani Nyamagana yatatengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
“Mji wa Usagara ndio mji uliotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza uchumi, hapa kutakuwa na biashara kubwa, hivyo jipangeni kutengeneza fedha na kufanya kazi,” anawahakikishia. Agizo la Rais kwa uongozi wa mkoa wa Mwanza kuhakikisha watu waliopora mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU) wanapatikana, ilikuwa habari njema kwa wakulima wa mkoani humo.
Kupitia hotuba yake, Magufuli aliweka wazi kwamba, NCU kwa sasa inashindwa kujiendesha kutokana na watu wachache kujitwalia mali zake kwa kuzinunua kwa bei ya hasara. Wamachinga ni kundi lingine ambalo Rais Magufuli aliwakoga kwa kugusia kero zao na kutoa tamko kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella akimtaka wasibughudhiwe. “ Mambo yenu (wamachinga) nayafahamu hata kabla sijafika hapa, niuombe uongozi wa Mkoa, Manispaa na Jiji upange ili kuona ni namna gani ya kuwapangia maeneo ya kufanyia biashara.
“Lakini kwa sasa wamachinga waendelee kukaa kwenye maeneo yao na ninyi mkielezwa mhame,” ni kauli ya Rais. Hata hivyo, aliwakumbusha wamachinga kutokuwa wakaidi kwa kuvunja sheria halali zilizowekwa na viongozi wa serikali na wale wa halmashauri kwa madai kuwa zinalenga katika kuboresha mambo muhimu ya nchi. Aidha, anawataka kutokubali kurubuniwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao huwapa bidhaa zao wawauzie kwa lengo la kukwepa kodi.
Anasema dhamira yake ni kuona wamachinga wanafanya biashara ili siku moja wawe wafanyabiashara wakubwa wanaolipa kodi. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alimshukuru Rais John Magufuli licha ya kuwa na ratiba ngumu ya kikazi lakini ameonesha mapenzi makubwa kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza na kufanya ziara ya kikazi. Mongella anamhakikishia Rais Magufuli juhudi walizoanza kufufua zao la pamba sanjari na kurudisha mali za NCU ambazo ziliporwa na baadhi ya watu.
Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula anamshukuru Magufuli kwa hatua mbalimbali za maendeleo zinazofanyika ikiwemo, uamuzi wake wa kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Airport, jijini Mwanza. Anasema ndani ya kipindi kifupi cha uongozi, Magufuli amefanya juhudi kubwa katika kutafuta fedha kwa ajili ya kuondoa kero za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wananchi. Kwa ujumla, ziara ya Rais Magufuli mkoani Mwanza, inaelezewa si tu na viongozi, bali pia na watu wa kawaida kuwa ilikuwa ya faraja na matumaini kwa wanyonge.
No comments:
Post a Comment