Thursday, August 18, 2016

Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi hospitali ya Mwananyamala Atumbuliwa

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mh Ally Hapi leo ametengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Delila Mushi kwa kosa la kupandisha bei ya baadhi ya huduma kinyume cha taratibu na sheria.

Mushi amedaiwa kupandisha bei ya huduma hizo baada ya kukaa kikao cha hospitali pasipo kuipeleka hoja ya kupandisha bei katika kikao cha Idara ya Manispaa na huduma za jamii.
Taratibu alizotakiwa kufuata Mushi ni kuipeleka hoja hiyo Manispaa, ambapo ingejadiliwa kwenye kikao cha huduma za jamii kisha baraza la madiwani kuipitia na kuitolea maamuzi jambo ambalo hakulifanya badala yake alipandisha bei pasipo kupitia taratibu hizo.

Bei ya huduma zilizopandishwa ni pamoja na bei ya kadi  ambapo wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo bila ya barua ya rufaa kutoka vituo vya afya na zahanati zilizo karibu nao, walitakiwa kulipa sh 10,000 badala ya 6,000.

“Hakuna jambo baya kama kiongozi kufanya maamuzi pasipo kufuata utaratibu halafu maamuzi hayo yakaathiri wananchi wanyonge, mkurugenzi nakuagiza hiyo bei ya kadi irudi kama ilivyokuwa awali, huwezi mlipisha mgonjwa kiasi kikubwa cha fedha huku huduma unazotoa haziendani na bei hiyo, ” amesema Hapi.

“Hakuna sababu ya anayekaimu nafasi ya mganga mkuu kwa sasa kubaki na wadhifa huo wakati haumtoshi, atatafutwa mwIngine kuja kuwa mganga Mkuu, ” amesema.

Kwa sasa ameteuliwa Dkt. Daniel Nkungu kukaimu kwa muda wadhifa huo hadi atakapoteuliwa mganga mwingine kushika wadhifa huo.

Hata hivyo, Baada ya Hapi kutoa agizo la kutenguliwa uteuzi wa Dkt. Mushi na kuamuru Wagonjwa kulipa bei ya kadi ya awali, baadhi ya wahudumu wa mapokezi waligoma kutoa huduma kwa madai kuwa mifumo ya utoaji risiti imeharibika.

Mariam Hamisi Sahabani mkazi wa Kinondoni, alifafanua jinsi wahudumu hao walivyogoma baada ya mkuu wa wilaya kuondoka.

“Baada ya Mheshimiwa kuondoka wamegoma kutoa huduma kwa kigezo kuwa mashine ilikuwa mbovu, inawezekanaje? Mbona wakati tunalipa 10,000 mashine zilifanya kazi, iweje sasa zisifanye? ” alihoji.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na wananchi waliokuwepo kwenye hospitali hiyo, Mganga mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Aziz Msuya alisema atawasimamisha kazi waliogoma kutoa huduma kwa kuwa walikuwa na lengo la kupinga kauli ya serikali.

“Naagiza huduma ianze kutolewa kuanzia sasa, na watakaogoma kutoa huduma nitawasimamisha kazi kuanzia kesho, ” amesema Msuya.

No comments:

Post a Comment