WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema shule za sekondari za kata zina fursa ya
kufanya vizuri kama zilivyo shule nyingine licha ya kuwa watu wengi
wamekuwa wakizidharau.
Ametoa
kauli hiyo jana mchana (Jumatatu, Machi 7, 2016) wakati akikabidhi
zawadi ya kompyuta mpakato (laptop) kwa mwanafunzi aliyeshinda shindano
la kuandika insha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC ). Kompyuta hiyo ina thamani ya sh. 1,992,000/-.
Mwanafunzi
huyo, Jabir Mandando (20), amehitimu kidato cha nne katika shule ya
sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa mkoani Lindi. Amepata
ufaulu wa daraja la pili na sasa anasubiri matokeo ya kujiunga na kidato
cha tano. Lakini aliandika insha hiyo mwaka jana wakati akiwa kidato
cha nne.
“Huyu
ni mtoto wa kijijini tu. Anatoka kijiji cha Namilema wilaya ya Ruangwa
mkoa wa Lindi. Shule ya Mbekenyera aliyosoma ni shule ya kata. Ameweza
kushinda tuzo na kushika nafasi ya tatu katika shindano lililoshirikisha
shule nyingi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
“Jabir
ameweza kuchomoza kitaifa kwa kushiriki shindano la kimataifa. Nimeamua
kumpa zawadi ya laptop pamoja na begi lake ili aweze kujisomea zaidi
na kupata elimu ya masuala mbalimbali kwa kutumia kompyuta hii. Pia
nataka iwe ni chachu kwa vijana wengine kushiriki mashindano kama haya,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu pia alikabidhi Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Shanael Nchimbi
fedha taslimu sh. 500,000/- zikiwa ni zawadi kwa ajili ya shule hiyo.
mwalimu Nchimbi alimsindikiza mwanafunzi huyo Arusha kupokea zawadi hizo
kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
uliomalizika Arusha wiki iliyopita.
Kwa
upande wake, kijana Jabir alisema anashukuru sana kwa zawadi aliyopewa
na kuahidi kuwa atajitahidi kusoma kwa bidii masomo ya kidato cha tano
na sita ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari.
Alipoulizwa alipataje taarifa ya uwepo wa shindano hilo, Jabir alisema: “Walimu
walipata taarifa wakazileta darasani na kutuambia tushiriki kuandika.
Walizikusanya na kuchagua tatu bora, ndipo yangu ikashinda.”
Amesema insha aliyoiandika ilihusu: “The importance of political stability in the East African Integration.”
Alimwonyesha
Waziri Mkuu cheti na dola za Marekani 200 ambavyo alipewa zawadi
kutokana na ushindi huo. Shule ya Mbekenyera ambayo alikuwa akisoma, pia
ilizawadiwa laptop na printer kutokana na ushindi wa kijana Jabir.
Mshindi
wa kwanza katika shindano hilo ametoka shule ya Sekondari Mzumbe,
mshindi wa pili alitoka Kenya na wa tatu alitoka shule ya Mbekenyera.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021, 11410 DAR ES SALAAM.
JUMATATU, MACHI 7, 2016.
No comments:
Post a Comment