Wednesday, March 2, 2016

Wakuu wa EAC kujadili marufuku ya mitumba

  Nguo za mitumba hutegemewa sana na watu wa mapato ya chini 

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana leo mjini Arusha, Tanzania moja ya mada za mkutano ikiwa kupiga marufuku uagizaji wa nguo za viatu vya mitumba.


Marufuku hiyo ni moja ya hatua zilizopendekezwa katika kuinua viwanda vya nguo katika kanda ya Afrika Mashariki.

Serikali za Afrika Mashariki zimekuwa zikilaumu uagizaji wa nguo na viatu vilivyokwisha kutumika kama moja ya sababu zinazofanya viwanda vya nguo na ngozi kusambaratika.

Nguo hizo hutegemewa sana na watu, hasa wa mapato ya chini kutokana na bei yake nafuu.
Kadhalika, hutoa ajira kwa maelfu ya watu ambao huhudumu kama wachuuzi.


Viongozi hao pia watajadili pendekezo la kupunguza kiasi cha magari yaliyotumika yanayoingizwa kanda hii, lengo likiwa kusaidia viwanda vya utengenezaji magari zinazoendesha biashara Afrika Mashariki.

Marais Paul Kagame (Rwanda), Uhuru Kenyatta (Kenya) na Yoweri Museveni (Uganda) tayari wamewasili Arusha kwa mkutano huo.

Maombi ya Sudan Kusini na Somalia kutaka kujiunga na jumuiya hiyo pia yatajadiliwa.

Wakati wa mkutano huo, viongozi hao wanatarajiwa kuzindua pasipoti ya pamoja ya Afrika Mashariki ambayo itakuwa katika mfumo wa elektroniki.

CREDIT:BBC

No comments:

Post a Comment