Friday, March 11, 2016
UJINGA USIO NA HASARA NI BORA KULIKO ELIMU ISIYO NA FAIDA "Life its all about Connection"
Na Mathias Canal, Dar es salaam
Ndugu zangu, Kuvaa Fulana, Jinsi na Raba kwangu mimi duh naona kama hata mwendo utabadilika ila rafiki zangu wengi wanatinga tu nami nasema tinga raba mwendo wa moka huwezi dunda.
Nianze kwa kuzitaja aina mbili za marafiki, Mosi ni ule urafiki ambao unatuama kwa shida na raha lakini pili niseme kuhusu urafiki wa kuchumia tumbo.
Urafiki wa kuchumia tumbo, hii ni aina ya urafiki ambao moja ya kijana, mzee au mtoto anamtumia mwenzake mahususi kwa mafanikio yake pekee pasina kujali umuhimu wa mafanikio ya mwenzake, Yaani unakuwa na rafiki ambaye hataki ufanikiwe anataka ubaki chini ili akutawale kiakili na uchumi, ukifanikiwa kwa kiasi tu anachachawa na mahaba pori.
Anaanza kuwa mnafiki, anakumbwa na chuki dhidi yako, anakusimanga kwa mabaya pekee, hawezi kukumbuka kwamba kuna magumu kapitia nawe ndiye uliyemsaidia kuvuka kwa kiasi hatua yake. Pengine niulize hivi kuna ubaya gani rafiki yako akiokota embe dodo kwenye mti wa Mwarobaini halafu akakuzawadia pia embe hilo, kwa kuwa una njaa kula embe kwanza ukishiba uliza iliwezekanaje kuokota embe kwenye mti usiozaa maembe.
Aina ya pili ya urafiki ni ule urafiki wa shida na raha, inafahamika vyema kwamba marafiki wazuri ni wale wanaosaidiana kwenye raha (Ndoa,Ujenzi,mafanikio yoyote yale) na kwenye shida (Kufiwa na mtoto, jamaa, rafiki au mtu wako wa karibu) ama jambo lolote lile gumu.
Huu hauwezi kuwa urafiki wa mashaka kamwe ndivyo ilivyo lakini ukipenyezwa unafiki, uzandiki, roho mbaya, chuki na ushirikina kidogo hakika hatua ya urafiki inakuwa imeanza kuingia doa na hatimaye kufa kabisa.
Jana nimepata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo ya takribani dakika 20 tu na rafiki yangu George David ambaye nimefanya nae kazi kwa takribani mwaka mmoja tukiwa kwenye lango la wanyang'anyi Ebony Fm, na sasa yupo East Afrika Radio iliyopo Dar es salaam dakika hizo zilitosha kabisa kujadili aina ya urafiki. Kila la kheri kijana haya ni mafanikio makubwa.
Kwa kawaida tu ili ufanikiwe unapaswa kukubali na kumuombea rafiki yako afanikiwe ili pia upate njia ya mafanikio zaidi, Na Tutambue tu hakuna Mafanikio bila Connection.
Wapo vijana wachache ambao wakiajiriwa na kuwa na mshahara wa laki nne pengine na viposho vya 450,000 ambavyo vinaleta hesabu ya laki 8 au 9 basi wanaona maisha ndo yamefika ukomo hakuna tena kufikiri zaidi.
Kuajiriwa sio pakuchekelea lazima utengeneze kipato kingine ili uwe na kiburi cha moyoni cha kukabili fedha zako, Ndugu yangu George David alinambia Ujinga usio na hasara ni Bora kuliko elimu isiyokuwa na faida hakika nilimuelewa sana.
"Life its all about Connection"
Naamini naeleweka vyema leo Neno La Wakati Mwema nimewiwa kidogo kusema kuhusu marafiki maana ndio maadui wa kesho kama tusipowaandaa vizuri katika urafiki mzuri wa badae. Lakini marafiki bora na muhimu ni wale wasiokuwa wahuni, ama walevi lazima iwe na marafiki wanaomcha Mungu itakujenga zaidi kuwa na hofu ya Mungu.
Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal
0756413465
Mabibo-Dar es salaam
No comments:
Post a Comment