WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atawatuma mawaziri watatu
waje mkoa wa Simiyu ili wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na
wananchi ili kubaini tatizo la mipaka baina ya wilaya hizo na Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti.
Waziri Mkuu
ametoa kauli hiyo jana(Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza na
mamia ya wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya akiwa kwenye siku ya
tano ya ziara yake mkoani Simiyu.
“Tangu niingie hapa mkoani malalamiko ya mipaka nimeyapokea kila mahali nilikopita. Nimeamua kuwatuma mawaziri watatu
ambao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William
Lukuvi; Waziri wa Maliasili ua Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene waje
mkoa huu kutatua matatizo yenu,” alisema.
“…Nitawatuma
waje na wapite kila wilaya, wakae na kuzungumza na wakulima na wafugaji
ili kubaini ni chanzo cha tatizo la migogoro hii kwenye mipaka ya
vijiji na hifadhi ya Serengeti. Pia Waziri wa TAMISEMI itabidi atoe
ufafanuzi kuhusu agizo lao la kutofanya shughuli yoyote mita 60 kutoka
kwenye mto Simiyu ili wananchi waelewe,” alisema.
Mapema, Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira) alimweleza waziri Mkuu
mbele ya wananchi hao kwamba limetolewa zuio linalowakata wakazi wa
mkoa huo wasifanye shughuli zozote umbali wa mita 60 kutoka kwenye kingo
za mto huo.
“Limebandikwa
tangazo linalokataza wananchi waishio kando ya mto Simiyu wasifanye
chochote kuanzia Julai 30, 2016. Wananchi hawajashirikishwa wala
kuelezwa chochote zaidi ya kuona bango la matangazo tu. Watu
wananakatazwa wasichote maji wala kunywesha mifugo wakati hakuna
mabwawa, itawezekanaje? Tunaomba kauli yako kuhusu jambo hili,” alisema.
Ili kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi
hapa nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali ina mpango wa kuunda mabaraza
ya ardhi 100 kwa nchi nzima ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati.
Akitoa
taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw. Erasto Sima
alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Julai mosi, 1987 ina ukubwa wa
kilometa za mraba 8,835 ambapo asilimia 49 (sawa na kilometa za mraba
4,329) ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori.
Alilitaja
eneo hilo kuwa ni pori la akiba la Maswa, sehemu ya hifadhi ya
Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na pori la hifadhi ya
usimamizi wa wanyama (WMA) la Makao na kwamba asilimia 51 iliyobakia
indiyo inayotumiwa kwa makazi ya watu, kilimo na malisho ya mifugo.
No comments:
Post a Comment