Thursday, March 17, 2016

Kiwanda Cha Rhino Cement Cha Tanga Chafungiwa Kwa Uharibifu Wa Mazingira


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina (MB) amekifungia kiwanda cha kuzalisha cement na chokaa kilichopo jijini Tanga cha Rhino Cement, jana jioni kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni uharibifu na uchafuzi wa mazingira na kuvunja sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.

Mh. Mpina amechukua uamuzi huo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kata ya maweni kupitia diwani wa kata hiyo Bw. Joseph Colvas na kujionea mwenyewe namna ambavyo kiwanda hicho kinavyo achilia moshi mzito kwenda angani, pamoja na vumbi lisilovumilika kusambaa katika maeneo ya makazi ya wanachi wa kata hiyo ikiwa ni pamoja na kusambaa katika maeneo ya shule ya sekondari ya Don Bosco ambapo, Mh. Mpina ameelezwa kuwa athari zitokanazo na uachiachi wa hewa hiyo chafu angani si tu kwa watoto wa shule zinazozunguka kata hiyo bali pia ni kwa viumbe hai na mazingira.

Kwa upande wake Afisa Afya wa jiji la tanga aliyejulikana kwa jina moja la bwana Kizito alimuelezea Naibu Waziri Mpina kuwa ni kweli kiwanda hicho kimekuwa kikifanya uchafuzi huo wa mazingira, na Afisa uendeshaji kutoka Baraza la Taifa na HIfadhi ya Mazingira NEMC Bw. Novatus Mushi ameeleza kuwa kiwanda hicho kimeshawahi kutozwa faini ya shilingi milioni kumi na saba (17) kwa kosa la kuchelewa kulipa ada ya mwaka ya mazingira pamoja na uharibifu wa mazingira uliokuwa ukifanywa na kiwanda hicho kwa upande wa kuzalisha chokaa.
 
Mh. Mpina ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC) kukifunga kiwanda hicho kisiendelee na uzalishaji kwa muda usiopungua miezi mitatu, na kulitaka baraza hilo lijiridhishe na kufuatilia namna kiwanda hicho kinavyotakiwa kutekeleza sheria ya mazingira kwa kujenga mfumo wa kisasa wa kutoa taka zitokanazo na uzalishaji kiwandani hapo pamoja, na kupima vumbi na moshi utokao kiwandani hapo kama hautakuwa na madhara na athari kwa mazingira na viumbe hai. Kinyume na hapo kiwanda hicho kitafungiwa moja kwa moja.
 
Aidha, akitolea mfano wa kiwanda cha bonite bottles cha mjini moshi kwa kuwa kinara katika upandaji miti na utunzaji wa mazingira, mh Mpina alivitaka viwanda vingine viige mfano wa kiwanda hicho cha coke cola.

No comments:

Post a Comment