Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Reli Tanzania TRL Kipallo Kisamfu (wa pili walioketi) na watendaji wengine wakiwa kwenye chumba cha mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar es salaam jana, baada ya kufikishwa kwa ajili kusomewa mashitaka yao dhidi ya tuhuma za ununuzi wa mabehewa feki ya kubebea kokoto ya kampuni hiyo
VIGOGO 11 wa Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kukiuka sheria wakati wa ununuzi wa mabehewa 25.
Washitakiwa hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu, Mkuu wa Kitengo cha Makenika na Mhasibu Mkuu Jasper Kisiraga; Kaimu Meneja wa Usafiri, Mathias Massae; Kaimu Mhandisi wa Ufundi na Meneja Ujenzi, Muungano Kaupunda na Mkuu wa Ufundi na Meneja Ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.
Wengine ni Mhandisi Mkuu wa Ufundi, Paschal Mafikiri; Mhandisi Mipango Kedmo Mapunda; Kaimu Mhandisi wa Mawasiliano, Felix Kashaingili; Mkuu wa Usafiri wa Reli, Lowland Simtengu; Mkuu wa Ubunifu na Utengenezaji wa Nyaraka, Joseph Syaizyagi na Kaimu Mkuu wa Usafirishaji; Charles Ndenge.
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Max Ali alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru jana kuwa, katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi 2013 na Juni 30, 2014 katika Makao Makuu ya TRL, Kisamfu akiwa mfanyakazi wa mamlaka hiyo, alitumia vibaya madaraka yake kwa kushindwa kusimamia vizuri zabuni kama ilivyokuwa inatakiwa kwenye vigezo na masharti.
Inadaiwa jambo hilo ni kinyume cha Sheria namba 21 ya Manunuzi ya 2004, jambo lililoipa faida kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industries Limited. Aliendelea kudai, kati ya Julai mosi na Agosti 31, 2013, Mafikiri alitumia madaraka yake vibaya kwa kuidhinisha michoro iliyoandaliwa na M/S Hindusthan, jambo ambalo ni kinyume na vigezo na masharti ya zabuni.
Kaunda anadaiwa alitumia madaraka vibaya kwa kuruhusu kutengenezwa kwa mabehewa 25, bila kuzingatia vigezo na masharti ya zabuni hiyo. Katika mashitaka mengine Kisiraga na Massae, wanadaiwa Agosti 5, 2014, walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Dola za Marekani milioni 1.3 bila kuthibitisha matumizi ya mabehewa 25, kupitia Cheti cha Ukaguzi na cha kukubali kinachotolewa na TRL baada ya kufanyiwa majaribio jambo ambalo ni kinyume na Sheria na kanuni za manunuzi.
Wakili Ari alidai katika mashitaka yanayowakabili Kaupunda, Mapunda, Kashaigili, Simtenguna Syaizyagi, kati ya Januari Mosi na Februari 2014, wakiwa wajumbe wa bodi ya zabuni hiyo, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuiruhusu M/S Hindusthan kushinda, ambayo ilikuwa haijakidhi vigezo kushinda zabuni hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kanuni za manunuzi.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na washitakiwa walikana mashitaka na kuomba wapewe dhamana. Hakimu Mchauru alisema dhamana ya washitakiwa ipo wazi endapo wataweka dhamana ya Sh milioni 10 pia wawe na wadhamini watatu ambao watasaini hati ya Sh milioni 10, wawasilishe hati zao za kusafiria mahakamani na wasisafiri nje ya mkoa bila kibali cha Mahakama. Kesi itatajwa tena Februari 25 mwaka huu.
CREDIT; HABARI LEO
No comments:
Post a Comment