
Mwalimu akitoa ushuhuda

Paulina
Mkonongo(wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Akisikiliza jambo


Mgeni
rasmi Bi. Paulina Mkonongo Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi akitembelea sehemu za maonyesho
kutoka kwa mashirika mbalimbali.

Baadhi ya wadau wakitembelea mabanda

Wadau mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake.
Maadhimisho
ya Siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake leo yamefunguliwa rasmi
kwa kuanza na maandamano ya amani yaliyoanzia uwanja wa Tipi Sinza
darajani hadi ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl iliyopo jengo la Ubungo
Plaza jijini Dar es salaam.
Maandamano
hayo yalihudhuriwa na maelfu ya watu yaliongozwa na bendi ya jeshi la
polisi kupitia njia za Shekilango kisha barabara ya Morogoro hadi katika
jengo la Ubungo Plaza ambapo yalipokelewa na Mkurugenzi wa shirika la
misaada la Marekani USAID Daniel
Moore, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Maire Matthews,
Mwakilishi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa Wanawake Lucy Melele,
Mkurugenzi wa shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani
Afrika - WiLDAF, Dr. Judith Odunga, pamoja na wawakilishi wa mashirika
wahisani na viongozi mbalimbali.
Akitoa
neno la ukaribisho, Dr. Judith Odunga alisema kampeni ya siku 16 kwa
mwaka huu imelenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama mashuleni.
Lengo kuu ikiwa kuhamasisha umma kuhusu ukubwa wa ukatili wa kijinsia
kwa vijana na watoto wetu mashuleni.
“Ni
kutokana na unyeti wa tatizo la ukatili wa kijinsia mashuleni, WILDAF
na wadau mbalimbali tumeona kuna umuhimu wa kushirikisha Wizara ya elimu
na ufundi stadi ili kuzungumzia ukatili wa kijinsia mashuleni na
kujenga mikakati ya kuzuia ukatili huo” Aliongezea.
Dr.
Odunga aliitaja kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni FUNGUKA! CHUKUA HATUA,
MLINDE MTOTO APATE ELIMU. “Kauli hii inalenga kumshawishi mtu binafsi,
kuwashawishi walimu, wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla, kuwalinda
watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha kwamba shule ni
mahala salama. Ni vyema kutafakari kwa kina jinsi vitendo vya ukatili wa
kijinsia mashuleni vinavyoathiri maendeleo ya watoto wetu kielimu.”
Alisema Dr. Odunga.
Dr. Odunga alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kufanya yafuatayo:
1. Kufutwa kabisa kwa adhabu ya viboko mashuleni na waalimu kufundishwa au kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2.
Kutengeneza mwongozo wa utekelezaji wa sera ya elimu ya mwaka 2014
utakaoelekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
3.
Kuboresha miundombinu rafiki ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwa na
madarasa ya kutosha, madawati, vyoo na sehemu za kujisitiri watoto wa
kike, mabweni, uzio pamoja na kuwa na usafiri wa uhakika kwa wanafunzi.
4. Serikali kuweza kuunda na kusimamia mabaraza yatakayo kuwa yanasikiliza malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5.
Tunaomba Wizara ya elimu na ufundi stadi kushirikiana na wizara ya
Katiba na Sheria na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
kutunga Sheria ya Ukatili wa Majumbani sambamba na kubadilisha Sheria ya
Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu ndoa kwa mtoto chini ya miaka 18.
Akifungua
rasmi kampeni hizi, mgeni rasmi Paulina Mkonongo ambaye ni Mkurugenzi
wa Elimu ya sekondari kutoka Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi
aliyemuwakilisha Katibu mkuu wa wizara hiyo alisema, “ukatili wa
kijinsia huleta athari hasi katika utoaji na upatikana wa fursa
mbalimbali za kijamii ikiwemo fursa ya elimu kwa watoto wetu, hivyo kuwa
ni kikwazo katika kujenga usawa wa kijinsia nchini.
Aidha
Mkonongo alisema serikali imefanya juhudi za makusudi kuzuia ukatili na
kuleta usawa katika kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kuweka sera na
mipango inayozingatia usawa na kupinga ukatili kwa makundi mbalimbali,
katika jamii ukiwemo ukatili wa kijinsia.
Mkonongo
alitoa wito kwa wananchi wote kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya
ukatili na kwamba kila mtoto ana haki ya kulindwa popote anapokuwepo iwe
nyumbani, shuleni, kwenye vyombo vya usafiri, michezoni na njiani
wanapokwenda na kurudi shuleni pia kuwapa mbinu za kujilinda wenyewe.
Naye
mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Bi. Maire Matthews alisema kuwa
takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wastani wa asilimia 45 ya
wanawake Tanzania wenye umri kati ya miaka 15 – 49 waliripoti kuwahi
kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono katika maisha yao. Alisema
takwimu nyingine zinakadiria kiwango hicho kuwa kati ya 41 – 56%.
Kwa
upande wake Lucy Melele kutoka shirika la UN Women aliyemwakilisha
Mwakilishi wa shirika hilo hapa nchini Anna Collins alisema wanawake na
wasichana ulimwenguni kote wanapitia aina mbalimbali za ukatili ambayo
inawanyima haki zao za msingi, ni tishio la demokrasia na ni kizuizi cha
amani ya kudumu. Hata hivyo alisema shirika la umoja wa mataifa
litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wa maendeleo, serikali,
mashirika mbalimbali, na jamii katika kampeni ya kupinga ukatili dhidi
ya wanawake na watoto.
Kampeni
ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia pia inafanyika kikanda katika
kanda ya ziwa (Mwanza, Mara na Shinyanga, kanda ya Kaskazini (Manyara,
Arusha, Kilimanjaro na Tanga), kanda ya kati (Dodoma, Morogoro na
Singida), kanda ya Kusini (Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa na Lindi, Kanda
ya Pwani (Dar es salaam na Pwani) zikisimamiwa na wadau mbalimbali
wakiwemo mashirika ya Kivulini, CWCA, NAFGEM, Morogoro Paralegal, Mtwara paralegal, WiLDAF, TWCWC pamoja na jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment