Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa
ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze
kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa
kishindo.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala
kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.
“Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura
nyingi za kutosha hata wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema
‘piga kura, linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”
Lubuva: Aeleze wanaibaje
Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) Jaji mstaafu, Damian
Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.
“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti
wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba,
vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu
aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”
Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu
na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga
ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina.
“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii
imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine
unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji
Lubuva.
Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na
baadaye kuteuliwa kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema
safari ya Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo
Watanzania watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza
undani kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.
Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka
wanawake nao kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa
wameshapika vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda
kura.
Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia
ya nchi kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”
Ukawa kutoyumba
Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema
Ukawa ipo imara haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu
kujipitisha kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.
“Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini
viongozi wapo imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya
ufukuzi ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa
Ukawa ikiingia madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha
wafanyabiashara kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.
“Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali,
Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela
zenu..tupo imara,” alisema.
MWANANCHI
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili
wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Madai hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku
tatu baada ya kujiuzulu uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za
kuachia nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kuhusu mgombea urais.
Akizungumza wakati akitangaza kujiuzulu wiki
iliyopita, Profesa Lipumba alisema dhamira yake ilikuwa inamsuta kwa kuwaingiza
ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi
kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.
Juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV
kutoka Kigali alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi
waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya
Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa
Ujenzi, Dk John Magufuli.
Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye
wiki mbili zilizopita alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi
ndani ya CCM ni mfumo alisema katika
kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha Ukawa, bali walikuwa tayari
wameparaganyika.
“Ukweli ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya
Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati
Ukawa tulikuwa na wagombea watatu… mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa
Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo
makubaliano hayo.
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa
apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti
kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi
hiyo kupiga hatua kubwa kiuchumi.
Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii
anatarajia kurejea nchini.
Agosti 6, mwaka huu Profesa Lipumba alijivua uenyekiti wa CUF wakati mkakati wa vyama vya
upinzani kushirikiana kushika dola ukiwa umeshika kasi.
MTANZANIA
WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni mgombea urais kwa
mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka
wananchi kuhamasishana na kumpigia kura ili apate ushindi wa asilimia 90.
Alisema akipata ushindi huo na hata kama Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kikiiba asilimia 10 ya kura zake, bado Ukawa watabaki na
asilimia 80 ambao ni ushindi mzuri.
Akizungumza na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa
makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni, Dar es Salaam jana, Lowassa
alisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuishinda CCM.
“Hawa jamaa ni hodari sana wa kuiba kura, tunahitaji
kufanyika kwa ushawishi na mshikamano, kila mtu anahitaji kushawishi wenzake
angalau watano ili tujihakikishie ushindi wa asilimia 90 pindi watakapoiba
asilimia 10 tutaibuka na ushindi wa asilimia 80.
“Ni bora tuhakikishe tunapata kura nyingi ili wakiiba
wasiweze kutufikia na jambo jingine tulinde kura zetu kama ambavyo sasa Chadema
wanafanya na CUF, wamekuwa ni bingwa wa kazi hiyo kwa muda,” alisema.
Alisema kama watahakikisha hilo linafanyika na
wanashikamana pamoja, itakuwa vigumu kwa CCM kuwashinda kirahisi katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Lowassa aliwaambia jambo muhimu wanalotakiwa kutambua
ni kutoyumba, kwani kwa kufanya hivyo watasababisha kujiwekea mazingira magumu
kuingia Ikulu na pia watambue kuwa kura ndiyo itawawezesha na si njia ya
maandamano hivyo aliwaomba kuhifadhi shahada zao.
“Hivi sasa Watanzania wapo makini na wapo tayari
kuongozwa kwenda Ikulu Oktoba 25, jambo la msingi ni kuhakikishi mnalinda
shahada zenu na kutumia nidhamu, tukitumia kura hawa tutawashinda Jumapili
asubuhi, hawana hoja tena washachoka,” alisema na kuongeza:
“Jambo muhimu ni kutoyumba, tukiyumba Ikulu mjue
hatuingii, huko tutaenda kwa kura na si kwa maandamano naomba sana mhifadhi
shahada zenu.”
UCHUMI
Lowassa, alisema miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa
yakimuumiza tangu akiwa CCM ni nchi kutosonga mbele kimaendeleo.
Alisema CCM imekuwa ikiendesha uchumi kwa tabu na
adha, jambo ambalo lilifanya kuwauliza wananchi kwamba wakati Mkapa anaondoka
madarakani dola ilikuwa shilingi ngapi na sasa ni ngapi? Wananchi wakajibu
ilikuwa 1,000 na leo shilingi 2,200 akawauliza je, huo ndio uongozi?
Lowassa aliwahoji tena, wakati Mkapa anaondoka
madarakani bei ya mchele ilikuwa shilingi ngapi? Wananchi wakajibu ilikuwa
1,000 leo imefikia shilingi ngapi? Wakajibu 2,500.
“Naweza kutaja vitu vingine vingi, niridhike kwa
kusema nachukia umasikini, nauchukia umasikini kwa akili yangu yote na ndiyo
maana naomba ridhaa kwa Watanzania niende Ikulu nikatoe umasikini kwa
Watanzania ili waweze kula milo mitatu, wawe na nyumba na gari la kutembelea,”
alisema.
“Kwa miaka 50 Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, alizungumzia kuhusu umasikini hadi leo bado tunazungumzia suala la
umasikini, maradhi na ujinga kwanini? Kwanini tunakubali kuendelea kuwa nyuma,
inabidi tufike mahali tujiulize kwanini Waganda, Wakenya, Wanyarwanda watupite
kwa uchumi.
Maandamano
Katika maandamano yanayotarajiwa kufanyika leo,
Lowassa alitoa wito kwa wanachama wanaounda Ukawa kuwa watulivu katika
maandamano watakayofanya kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu
ya kugombea urais.
Maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia katika ofisi za
chama hicho na kwenda ofisi za Chama cha NCCR- Mageuzi na baadaye NEC kuchukua
fomu na wakishachukua wanamalizia ofisi za Chadema ambapo viongozi wa Ukawa
watazungumza na wananchi.
“Kumbukeni maadui zenu huwa wanasema chama chetu kina
fujo eti hakina heshima kwa akina mama na wazee, hivyo naomba tujihadhari na
maneno hayo na katika maandamano ya leo tuwe na nidhamu na waungwana na
tusikilize maelekezo ya Serikali, hawa wanataka kutuzingua hivyo tusiwaruhusu
watuzingue,” alisema.
“Kwa kupitia umoja wetu tujue kwamba tusipochukua
Ikulu mwaka huu itatuchukua miaka 50 ijayo, hivyo nawapeni pole kwa kujiuzulu
kwa mwenyekiti wenu,” alisema.
“Ukawa kuna viongozi hodari na imara kwani wamepitia
misukosuko mingi sana, lakini wameishinda kwa umoja na mshikamano wangeyumba
wangechukulia poa.
“Ukawa ina Mwenyekiti wake, Emanuel Makaidi,
Mwenyekiti Freeman Mbowe, James Mbatia ambaye anajua Qur’an na Biblia na Maalim
Seif ni hodari sana wa kupatanisha watu na ni mpambanaji asiyekata tamaa
nimepata faraja kujiunga nao,” alisema.
POLE YA KUONDOKA LIPUMBA
Lowassa pia alitoa pole kwa wanachama wa CUF kwa
kuondokewa na mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, ikiwamo na kuwapongeza
kwa namna walivyolikabili jambo hilo.
“Tatizo la Afrika viongozi wanatumia mamlaka kienyeji
sana, wamekuwa wanatengeneza Katiba kwa kuwarejesha madarakani ila hapa
tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kushirikiana na kuwa na umoja,” alisema.
Alisema mwaka 1995, Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Nyerere
alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM aliwaambia wanachama wa chama hicho
kwamba, ‘watu wengi wanataka mabadiliko hivyo wasipoyapata ndani ya CCM
watayatafuta nje ya CCM’.
Baada ya kusema maneno hayo, Lowassa alitoa kauli
mbiu yake inayosema ‘safari ya mabadiliko wananchi wakajibu ‘nje ya CCM’.
Alisema ujio wake Ukawa, ni kutekeleza maagizo ya
Mwalimu Nyerere ya kumtaka kutafuta mabadiliko nje ya CCM ikiwamo na kuandika
historia ya nchi ambayo inawezekana.
“Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia
tuli…wasiwadanganye kwani tupo imara na Mwenyezi Mungu atatusaidia, kwani
wanajaribu kupitisha fedha lakini wajue kuwa viongozi wa Ukawa hawahongeki,”
alisema.
MTANZANIA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Arusha, Onesmo Ole Nangole na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mkoa huo, Isack
Joseph, wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ole Nangole na Joseph walifikia uamuzi huo jijini
hapa jana na kusema kwa nyakati tofauti wamelazimika kuchukua uamuzi huo kwa
kuwa utaratibu wa kumpata mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulikiukwa.
Kwa mujibu wa wana CCM hao, wakati wa mchakato huo
baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho walikuwa na wagombea wao mifukoni
waliotaka wagombee nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Ole Nangole aliyejiondoa CCM akiwa
kwenye kipindi cha awamu ya pili cha uenyekiti wake, alisema alijiunga CCM
mwaka 1977 ambapo alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo mwenyekiti
wa CCM wilaya kwa miaka kumi.
“Ndugu zangu waandishi wa habari nimewaita leo
kuwaambia jambo moja kwamba ninahama CCM kuanzia sasa. Najiuzulu nafasi yangu
ya mwenyekiti niliyoitumikia kwa miaka saba na ninajiunga na Chadema kuanzia
sasa.
“Nashindwa kuwa na moyo wa chuma wa kuendelea kuwa
ndani ya CCM kwa sababu CCM niliyoifahamu tangu enzi za TANU siyo hii ya sasa.
“Kuondoka kwangu kumechangiwa na kikundi cha viongozi
wachache kuiongoza CCM kwa mabavu, nguvu na kwa kutumia fedha walizokwapua
serikalini.
“Miaka yote tangu nilipojiunga CCM mwaka 1977,
sikuwahi kukiona chama hiki kikiendesha mambo yake bila kufuata kanuni na
taratibu za vikao kama kilivyofanya wakati wa vikao vya kupitisha mgombea urais
mjini Dodoma hivi karibuni.
“Mkutano mkuu wa CCM uliongozwa kwa kukiuka haki na
misingi kwa wanachama kwani hata nyinyi mtakumbuka kulikuwa na mchakato wa
urais na wagombea 40 walijitokeza akiwamo Edward Lowassa.
“Kwa mapenzi yake Lowassa alivyokitumikia chama na
Taifa, wananchi tuliamini mchakato ule kama jina lake lisingekatwa angekuwa
mmoja wa wagombea ambao wangefika mbali ndani ya chama.
“Lakini jina lake lilikatwa bila sababu japokuwa
sababu tulizijua tangu alipotoka kwenye uwaziri mkuu kwa vile kuliendelea
kusambazwa maneno na hujuma za kisiasa dhidi yake kupitia kwa viongozi wa chama
na Serikali wakiwamo vijana wadogo waliopewa fedha na madaraka ili wamchafue,”
alisema Ole Nangole.
Kwa upande wake, Joseph alimnyooshea kidole Katibu wa
CCM, Abdulrahman Kinana na kumtaka achunge ulimi wake pindi anapowaita
Watanzania makapi ndani ya nchi yao.
Joseph ambaye ni Diwani wa Kata ya Monduli Mjini
aliyemaliza muda wake na kupita bila kupingwa ndani ya CCM, alisema hakuna
Mtanzania aliye makapi kwani wote wana haki ya kidemokrasia ya kuhama vyama kwa
jinsi watakavyoona inafaa.
“Watasema mengi na tumeondoka watatuita makapi.
Naomba niwaambie, sisi siyo makapi, wakitaka tuzungumze suala la makapi hao
wanaosema hivyo wao ndio makapi halisi.
“Sisi Watanzania si makapi kwani tukichambuana kwa
suala la makapi na kuangalia wewe umetokea wapi, tutakwenda kusiko. Kwanza
aliyesema hiyo kauli yeye ni Msomali. Hivyo tukisema nani ni makapi yeye ndiye
makapi halisi anayeishi Tanzania kwani asili yake ni Somalia,” alisema Joseph.
Joseph alitoa kauli hiyo zikiwa ni siku chache baada
ya Kinana kunukuliwa na vyombo vya habari akisema wanachama wa CCM wanaohamia
Chadema ni makapi.
Akizungumzia kuhusu kuhama kwake, alisema ametafakari
kwa muda kilichotokea mjini Dodoma na kisha kuamua kuiridhisha roho na nafsi
yake, kwamba kilichofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM kilikuwa ni uhuni wa
kisiasa.
“Mheshimiwa Lowassa alisema demokrasia imebakwa ndani
ya CCM. Mimi nasema kanuni na taratibu za CCM zimehodhiwa na kikundi cha watu
wachache.
“Ukiona wachache wanahodhi madaraka ya chama, huna
sababu ya kurudi nyuma na kuangalia chama ni cha watu wachache au ni cha
wanachama.
“Hivyo basi, nimetafakari kwa muda mrefu, nimeridhika
kwamba uamuzi ninaouchukua kuondoka CCM na kujiunga na Chadema ni sahihi,”
alisema Joseph.
MTANZANIA
JOTO la uteuzi wa mwisho la kupata wagombea ubunge
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) limezidi kupanda, huku chama hicho
kikitangaza uamuzi mgumu kwa wagombea waliocheza rafu na hata kupindua matokeo.
Mbali na hayo, viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa
wanaodaiwa kuwabeba kinyume na utaratibu nao wapo hatarini kuvuliwa nyadhifa
zao.
Taarifa kutoka ndani ya CCM zililiambia MTANZANIA
jana kuwa kikao cha Sekretarieti kilichokutana mjini hapa, kilijadili baadhi ya
taarifa na rufaa za wagombea, huku wengine wakiwalalamikia wenzao pamoja na
viongozi kwa kucheza rafu wakati wa uchaguzi wa kura za maoni.
Miongoni mwa jambo ambalo limekuwa likizua mjadala,
ni hatua ya baadhi ya wabunge kupata kura nyingi katika maeneo yao kinyume na
idadi halisi ya wanachama wa CCM kwenye jimbo husika.
Moja kati ya majimbo ambayo wagombea walilalamikia
hatua hiyo, ni Jimbo la Iramba ambapo Juma Kilimbah ambaye alikuwa ni moja ya
wagombea, alisema pamoja na kura kupigwa bado kura alizopata mgombea mwenzao,
Mwigulu Nchemba ni tofauti na idadi ya wapiga kura.
Alidai wakati wa mchakato huo, baadhi ya viongozi wa
CCM akiwemo msimamizi wa uchaguzi, walikuwa wakigawa kadi kinyume na utaratibu
kwa lengo la kumwezesha Mwigulu kushinda.
Akizungumza mjini hapa, Katibu wa NEC, Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye, alisema vikao hivyo vilivyoanza jana vinaweza kutengua
ushindi wa wagombea hao.
Alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji
wa kanuni za uchaguzi katika upigaji wa kura za maoni.
“Pamoja na uchaguzi kumalizika ni lazima wana CCM
watambue kuwa kulalamika pembeni au katika vyombo vya habari hakusaidii, ni
lazima wafuate utaratibu wa chama.
“Kikubwa wanachama wawe watulivu na vikao hivi
vitachambua kwa kina kila tukio katika kila jimbo, wilaya na hata mkoa kabla ya
kuteua jina la mgombea wa ubunge kwenye jimbo husika,” alisema Nape.
NIPASHE
Baada kimya cha muda mrefu hatimaye Katibu Mkuu wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilibrod Slaa, anatarajiwa
kufungua pazia la kampeni za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Imeelezwa kuwa, Dk. Slaa ambaye kwa sasa amepewa
likizo na chama chake baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiunga
na chama hicho, atafungua kampeni za Ukawa mkoani Dar es Salaam mwezi huu.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zitaanza rasmi
Agosti 22, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu
Mkuu Bara wa Chadema, John Mnyika, alidokeza kwamba Dk. Slaa atazindua kampeni
za Ukawa katika Jimbo la Kibamba, ambalo yeye (Mnyika) anagombea ubunge kwa
tiketi ya umoja huo.
Mnyika alidokeza hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza
na viongozi wa matawi na kata ya Goba, muda mfupi kabla ya kufanyika uchaguzi
wa kura za maoni kumchagua mgombea udiwani katika eneo hilo.
“Dk. Slaa yupo mapumzikoni na jana nilizungumza naye
kwa kirefu na aliniambia bado anapumzika, lakini atakuja kushiriki kampeni
Jimbo la Kibamba ambalo mimi nagombea ubunge,” alisema Mnyika.
Hata hivyo, Mnyika alipoulizwa kama Dk. Slaa
atashiriki kampeni za nchi nzima ama ataishia Jimbo la Kibamba pekee kama
alivyozungumza naye, Mnyika hakutaka kufafanua zaidi.
Katibu huyo wa Chadema hajashiriki katika shughuli
mbalimbali za Ukawa ikiwamo kikao cha Ukawa cha kumkaribisha Lowassa kwenye
makao makuu ya Chama cha Wananchi (Cuf), mapokezi ya mwanasiasa huyo na mkutano
mkuu wa Chadema uliompitisha kugombea urais kupitia Ukawa.
Hata jana Dk. Slaa hakuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu
la Taifa la Cuf ambao ulihudhuriwa na viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda
Ukawa vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD.
Waliohudhuria jana ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe; Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Dk.
Emmanuel Makaidi.
Pia walikuwapo wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano,
Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea
mwenza, Juma Haji Duni.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chadema wiki
iliyopita, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, Dk. Slaa kwa sasa
yupo mapumzikoni, lakini kampeni zitakapoanza ataongoza kampeni za Ukawa kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwa ngazi ya
udiwani, ubunge na urais.
Mnyika aliwaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa Ukawa
utashinda uchaguzi huu na kwamba kinachotakiwa ni wao kujiandaa kufanya kampeni
za nguvu ili kuwafikia wananchi wengi.
Hata hivyo, Dk. Slaa alipotafutwa jana kuthibitisha
maelezo ya Mnyika, simu yake ya mkononi haikupatikana.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms)
hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Katika kura za maoni kata ya Goba, viongozi wa matawi
na kata walimchagua, Rick Ambinga, kupeperusha bendera ya chama hicho katika
nafasi ya udiwani.
Ambinga aliwashinda wagombea wenzake wanne katika
uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Katibu wa Jimbo la Ubungo, Justin Mollel.
Habari za Dk. Slaa kuzindua kampeni za Ukawa kama
zitakuwa ni za kweli itakuwa faraja kwa wafuasi na viongozi wa vyama
vinavyounda Ukawa.
Wiki iliyopita zilivumishwa taarifa za uvumi zikidai
kuwa kiongozi huyo angerejea katika ofisi za Chadema kuendelea kuchapa kazi,
hali iliyowalazimisha baadhi ya wafuasi wa Chadema kwenda katika ofisi hizo,
lakini walielezwa na viongozi kuwa hazikuwa habari za kweli.
Alhamisi iliyopita, Ukawa ilipata mtikisiko, baada ya
Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba, kutangaza kujiuzulu akidai kuwa
amechukua uamuzi huo kutokana na kuonekana kuwa kikwazo katika baadhi ya mambo
ndani ya Cuf na kwamba roho yake imemsuta asikubaliane na uamuzi wa Ukawa wa
kumpokea Lowasa na kumpa fursa ya kugombea urais kupitia Ukawa.
HABARILEO
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa
amekanusha uvumi kuwa ameungana na wenyeviti wengine wa mikoa wa CCM kukihama
chama tawala nchini. Amesema wanaomzushia washindwe na walegee, kwani moyo na
mwili wake upo CCM na kwamba kamwe hawezi kuhama.
Aliyasema hayo jana mjini hapa kutokana na kuwapo kwa
taarifa amekihama chama hicho. Awali, jana kulikuwa na taarifa za Mwenyekiti wa
CCM mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole kuhamia Chadema, kama ilivyokuwa kwa
Mgana Msindai, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida aliyetangulia
Chadema wiki iliyopita baada ya kushindwa kura za maoni ndani ya CCM.
Katika kuthibitisha hayo, Kimbisa jana alikuwa
akiendesha vikao vya Kamati ya Siasa ya Mkoa akiwa katika sare zake za chama.
Taarifa hizo zimekuja huku Kimbisa akiwa na habari nyingine katika gazeti hili
(ukurasa wa 21) akielezea kushangazwa na wanaokihama chama baada ya kushindwa
katika michakato ya kuwania uongozi, huku akisema kamwe yeye hawezi kufanya
hivyo.
“Mwaka 2010 niligombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini
nikahesabu kura zangu mwenyewe nyumbani nikajiona nimeshinda nikalala, asubuhi
nilipoamka kumbe wagombea wenzangu wakaunganisha matokeo yao mgombea mmoja
akaonekana ameshinda, lakini bado sikuhama na hadi leo nina damu ya kijani.
“Mtu akihangaika kuondoka CCM baada ya kushindwa
tutamfuata hukohuko na tutampiga kwa kura tu,” alisisitiza Kimbisa.
No comments:
Post a Comment