Saturday, July 4, 2015
Boko Haram waua watu 200 katika kipindi cha siku mbili
Kundi la kitakfiri la Boko Haram limeua karibu watu 200 katika mashambulizi yao mapya dhidi ya nyumba na misikiti nchini Nigeria kwenye kipindi cha siku mbili zilizopita. Mapema jana Ijumaa, wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi waliowatoa kwa nguvu watu wapatao 11 kwenye nyumba zao katika kijiji cha mbali cha Miringa kwenye jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuwaua mbele ya wanavijiji wengine. Shirika la habari la Ufaransa limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, watu hao wanadaiwa kukataa kushirikiana na kundi hilo la kigaidi. Mkazi mmoja wa kijiji hicho amenukuliwa akisema kuwa, watu hao walikimbia nyumba zao katika kijiji cha Gwargware katika jimbo la Yobe na kujificha kwenye kijiji hicho cha Miringa. Katika tukio jingine la umwagaji damu, kundi la wanamgambo zaidi ya 50 wenye silaha waliokuwa wamepanda pikipiki walikivamia kijiji cha Mussa katika jimbo la Borno na kuwapiga risasi kiholela wakazi wa kijiji hicho na baadaye kuwachomea moto nyumba zao. Jana hiyo hiyo pia, msichana mmoja mwenye umri wa miaka 15 alijiripua kwa mabomu katika msikiti mmoja kwenye kijiji kingine cha Borno yaani kijiji cha Malari na kuua Waislamu 12 waliokuwa wakisali msikitini humo
No comments:
Post a Comment