Thursday, July 16, 2015

Aliyepigwa risasi nane azinduka, ataja ‘muuaji


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus SabasKamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas


MKAZI wa eneo la Kanisani, Kata ya Sokon One mjini hapa ambaye alipoteza fahamu kwa zaidi ya wiki na kulazimika kupumua kwa msaada wa mashine katika Hospitali ya Selian alikokuwa amelazwa baada ya kupigwa risasi nane, amezinduka na kutaja jina la mmoja wa wabaya wake.

Godson Ruwaichi, ambaye bado yuko chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini hapo, hawezi kuzungumza vizuri, lakini amefanikiwa kuwaeleza ndugu zake jina la mwanamke anayedhani alihusika na kutekwa kwake wiki iliyopita wakati akitokea kazini eneo la Sakina, kuelekea nyumbani Sokon One.

Inadaiwa watu wasiojulikana walimteka nyara na kumpeleka kwenye nyumba isiyojulikana ambako dakika chache kabla hajapigwa risasi, alisikia sauti ya kike ikiwafokea watekaji kuwa “Huyu siyo yeye, mmekosea sana kumleta mdogo wake,” na baada ya hapo alipoteza fahamu.

Madaktari katika hospitali ya Selian wameeleza kuwa Godson alipigwa risasi nane na watekaji wake ambao baadaye waliutupa mwili wake barabarani kabla kuokotwa na wasamaria wema na kwamba mgonjwa wao huyo ameweza kuishi kwa bahati tu.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa tayari jeshi lake limeanza uchunguzi wa kisa hicho na linawashikilia baadhi ya watuhumiwa wa sakata hilo, kutokana na maelezo ya Godson.

No comments:

Post a Comment