Papa msofe
Hata hivyo, baada ya kuachiwa, Msofe alikamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.
Hakimu Mkazi, Renatus Rutta aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya kufuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Kesi hiyo imefutwa kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) aliwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao. Msofe na Makongoro wamesota rumande kwa zaidi ya miaka miwili kwa kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa unadai upelelezi wa kesi haujakamilika.
Msofe kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani, Agosti 2012 na Makongoro Februari 2013. Baada ya kuachiwa Makongoro aliruhusiwa kuondoka katika eneo la mahakama na Msofe alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Rutha na kusomewa mashitaka mawili.
Katika mashitaka hayo, Msofe anadaiwa Desemba 23, 2004 katika Wilaya ya Ilala kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka ya kuhamisha haki ya umiliki wa nyumba namba 288 ambayo ni mali ya aliyekuwa mfanyabiashara wa madini, Onesphory Kituli (sasa marehemu).
Ilidaiwa kuwa Msofe kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka hiyo akionesha Desemba 13, 2004 Kituli alihamisha haki yake ya umiliki wa nyumba hiyo kwake wakati akijua ni uongo.
Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Desemba 23, 2004 na Machi 30, 2005 kwa nia ya kudanganya, Msofe alitoa nyaraka hizo za uongo kwa Kamishna wa Ardhi kwa lengo la kuhamisha umiliki kutoka kwa Kituli kwenda kwake.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na dhamana kwa mshitakiwa ipo wazi endapo atatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni 10 kila mmoja. Kesi itatajwa tena Julai 9, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment