WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema CCM ni chama pekee nchini ambacho kimefanikiwa na kinaendelea kupanua wigo wa demokrasia.
Nyalandu ni miongoni mwa wanachama wa chama hicho nchini waliotia nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao, aliyasema hayo jana wakati anazungumza na viongozi na wanachama wa CCM wilayani Masasi waliojitokeza kumdhamini.
Alisema hakuna tunu bora nchini zaidi ya kuendeleza umoja, amani na mshikamano uliopo hivi sasa ndani ya chama hicho huku akitoa mwito kwa wagombea wenzake ndani ya chama kuacha kukitia madoa chama na hata wao wenyewe, kwani kwa sasa CCM inahitaji umoja.
Alisema wana CCM nchini waondoe tofauti zao kwa kuwa ndiyo silaha pekee itakayoirudisha madarakani ambapo pia aliwaasa watanzania kupinga vitendo vyote vya kibaguzi, udini, ukabila na hata tofauti za rangi na kwamba endapo CCM kitampa ridhaa ya kuwa mgombea wa urais atahakikisha vitendo hivyo vinabaki kuwa historia.
Kwa mujibu wa Nyalandu, amekuwa CCM kwa muda mrefu sasa na kwamba kwa sasa Mungu ameruhusu kizazi kingine kipate fursa ya kuongoza nchi lengo likiwa ni kujenga uchumi imara kwa kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo gesi, mafuta, milima pamoja na hifadhi za Taifa.
No comments:
Post a Comment