Friday, June 26, 2015
Dk Shein kuvunja Baraza la Wawakilishi
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein leo anahutubia Baraza la Wawakilishi, akitarajiwa kutumia fursa hiyo kuaga na kusitisha uhai wa Baraza hilo uliodumu kwa miaka mitano na hivyo kumaliza kazi yake kwa mujibu wa Katiba.
Hata hivyo, Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, amezuiwa kuingia baada ya wajumbe wa Baraza hilo kukataa kutoa kibali cha kumruhusu kuongozana na Dk Shein katika shughuli hiyo ya kuvunja baraza.
Maamuzi ya kumkataa Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, yalifikiwa jana na wajumbe hao baada ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kuwataka kuridhia kutolewa kibali kwa wageni atakaofuatana nao Dk Shein na kuingia nao ukumbi wa Baraza.
Kificho alisema Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ni sehemu ya Baraza la Wawakilishi, lakini atafuatana na baadhi ya viongozi na wasaidizi wake ambao wanatakiwa wapate idhini ya ruhusa kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Baadhi ya watu maarufu ambao Spika aliwataja, wanahitaji idhini kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuingia ukumbi wa baraza wakati rais akihutubia ni pamoja na Msaidizi wa Rais na Jaji mkuu wa Zanzibar ambapo wajumbe wote walikubaliana na kusema wanaridhia ujio wao.
Kificho aliendelea na kumtaja mgeni mwingine kuwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ambapo wajumbe kwa kauli moja walipinga na kusema hawataki kuona anaingia katika ukumbi huo.
Akifafanua baada ya msimamo huo wa wajumbe, Kificho alisema; ‘’Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nyinyi ndiyo wenye idhini ya kumtaka mtu gani ahudhurie ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi...... tayari nilikuwa nimemwandikia barua Maalim Seif kuhusu kuhudhuria kikao hicho, lakini kwa kuwa mmekataa basi nitamuandikia barua nyingine kuhusu mabadiliko na kumuambia kwamba asije tena kwa sababu wajumbe wamekataa,” alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM walifurahia uamuzi huo ambao unakwenda sambamba na wajumbe kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kuendelea kususia kikao cha Baraza la Wawakilishi.
Hatua hiyo imeibua hofu na wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya kisiasa Zanzibar pamoja na uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa zaidi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ambapo kwa kawaida joto la kisiasa huzidi kupanda.
Kwa uamuzi huo, Dk Shein anatarajiwa kulihutubia Baraza la Wawakilishi bila ya wajumbe kutoka CUF ambao wameendelea kususia kikao, kutokana na madai yao kwamba wananchi wananyimwa haki na fursa ya kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura kupitia mfumo wa kisasa wa kielektroniki wa BVR.
Uandikishaji Akizungumzia uandikishaji kwa mfumo wa BRV, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud aliwataka wananchi wenye sifa wajitokeze kujiandikisha kwa ajili ya kutekeleza matakwa ya kisheria kupiga kura kwa watu wenye sifa na vigezo vya kupiga kura katika chaguzi mbalimbali.
“Si kweli kwamba uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura unafanyika kwa ubaguzi na upendeleo kwa aina ya watu... wenye sifa wajitokeze na kuandikishwa,” alisema.
CREDIT: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment