METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 28, 2021

WAZALISHAJI NA WAFUNGASHAJI WA BIDHAA MKOA SINGIDA WAPEWA ELIMU YA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI




 

Wazalishaji na Wafungashaji wa bidhaa katika Mkoa wa Singida watakiwa kuzingatia elimu ya  matumizi sahihi ya  vipimo ili waweze kurudisha imani kwa watumiaji wa bidhaa zao na  kuimalisha masoko ya ndani na nje ya nchi  na hivyo kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. 


Ameyaeleza hayo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi wakati wa akifungua Mkutano wa utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa wazalishaji na wafungashaji wa bidhaa ulioandaliwa na  Wakala wa Vipimo (WMA) katika ukumbi wa Bishop Rwoma – Singida mjini leo Aprili 28, 2021.

 

‘‘Elimu ya matumizi ya vipimo sahihi itakayotolewa leo itakuwa msaada mkubwa kwetu sote na Taifa kwa ujumla ukizingatia tunatumia vipimo kufanikisha mambo mbalimbali yanayotuzunguka; iwe kwenye ujenzi, afya, mazingira, usalama na katika maeneo tuliyozoea ya kibiashara na bidhaa za mkoani kwetu zitakuwa na vipimo sahihi vitakavyorudisha imani kwa watumiaji wa ndani na nje na kuimalisha soko la bidhaa zenu’’ ameeleza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi.

 

Dkt.Rehema Nchimbi ameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kuendelea kutambua wajibu wao wa kuendelea kuwatembelea na kuwafikia wananchi kwa kusogeza elimu na mafunzo ya matumizi sahihi ya vipimo katika Mkoa wa Singida na hivyo, amewataka kuendelea kutoa elimu  kwa wazalishaji na wafungashaji kila inapobidi ili kuwaondolea vikwazo kwenye shughuli zao za kila siku  katika Mkoa wa Singida  ili Mkoa uweze kuwa mfano  katika matumizi ya vipimo sahihi.


 

Aidha, Dkt.Rehema Nchimbi ameziagiza  halmashauri na manispaa kutenga jengo ambalo litakuwa ni kituo cha kutoa huduma zote kwa wananchi wote ambao ni wazalishaji na wafungashaji  ikiwemo huduma ya  vipimo  na huduma nyingine zinazowiana ili wananchi wanapokuja waweze kupata huduma zote sehemu moja.

 

Dkt.Rehema Nchimbi ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa mfano katika kutekeleza masuala yote yanayohusiana na vipimo watakayofundishwa na baada ya mafunzo hayo, bidhaa za Mkoa wa Singida ziwe na vipimo sahihi vitakavyorudisha imani kwa watumiaji wa ndani na nje na kuimalisha soko la bidhaa zenu za Mkoa na nchi kwa ujumla.




 Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Wakala wa Vipimo Bw. Deogratias Maneno ameeleza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa utoaji wa elimu ya vipimo katika Mikoa yote nchini na kwa Mkoa wa Singida yamelenga kutoa elimu ya vipimo kwa wazalishaji, wafungashaji, wauzaji wa mafuta ya alizeti, unga pamoja na  wasindikaji wa asali.

 

Bw. Deogratias Maneno ameeleza kuwa kipimo sahihi ni nyenzo muhimu katika kubadilishana bidhaa na fedha, ili biashara ifanyike kwa haki lazima vipimo sahihi vitumike, mfano mtu anayefungasha bila kufuata matakwa ya Sheria ya Vipimo anaweza kuzidisha au kupunguza ujazo/uzito wa bidhaa. Kuzidisha vipimo kunampa hasara mwenye mali (mtengenezaji) na kumfanya asipige hatua katika biashara yake, wakati kupunguza kunasababisha mnunuzi kupata bidhaa pungufu ya pesa aliyotoa.

 

Naye, Maliam Mohamed, Mjasiliamali kutoka Ikungi Singida ameshukuru Wakala wa Vipimo kwa elimu waliyoitoa kwao ambayo itakuwa msaada mkubwa katika biashara zao na itawasaidia kufanya biashara kwa uaminifu, uhuru na kujiamini na hiyo itawafanya kusafirisha bidhaa katika Mikoa mingine kwa sababu  watakuwa na uhakika wa vipimo sahihi na itawasaidia  kuondokana na  adhabu ya faini au kifungo kama Sheria ya vipimo inavyosema.





Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com