Wednesday, October 25, 2017

Vilaza 1,194 wachaguliwa sekondari Ukerewe

 Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Estomiah Chang'ah

WANAFUNZI 1,194 wasio na sifa wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, walichaguliwa kwenda sekondari mwaka 2015 wakati hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Frank Bahati. Amesema uchunguzi unaendelea dhidi ya walimu wote waliohusika kuvujisha mtihani wa darasa la saba mwaka 2015.

Kwamba uchunguzi utakapokamilika, watachukuliwa hatua za kisheria. Alisema hayo katika kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika jana mjini Nansio, kujadili na kuweka mikakati kukabili tatizo la wilaya hiyo kuendelea kufanya vibaya kitaaluma.

Bahati alisema hatakuwa na huruma kwa walimu wanaokiuka maadili ya kazi. Alieleza kuwa katika uchunguzi aliofanya, amebaini walimu wakuu 72 wa shule za msingi na waratibu elimu kata 18, walihusika kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2015, hivyo kusababisha wanafunzi 1,194 wasio na sifa wachaguliwe na kwenda sekondari wakati hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mwaka 2015 Ukerewe ilikuwa ya kwanza mkoani Mwanza kwenye wilaya za Buchosa, Magu, Misungwi, Sengerema, Ilemelana Nyamagana wakati kitaifa ilishika nafasi ya tano kati ya shule za msingi 186.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Estomiah Chang’ah aliitisha kikao hicho kujadili na kuweka mipango ya kuikwamua kitaaluma, baada kuwa ya mwisho kati ya wilaya saba za mkoa wa Mwanza kwa mara ya pili mfululizo katika matokeo ya darasa la saba, yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ofisa Elimu Msingi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Reonard Richard alisema jumla ya wanafunzi 10,042 walifanya mtihani huo mwaka huu, lakini waliofaulu ni asilimia 50.7, hivyo kushuka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na ufaulu wa asilimia 62.1 wa mwaka uliopita.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kakerege, Deus Tibalemwa alisema udanganyifu wa mitihani uliofanyika huko nyuma, ndio sababu ya walimu kufanya kazi kwa mazoea na kuacha kujituma, hivyo kusababisha anguko la kitaaluma linalotokea sasa, baada ya kuwepo usimamizi mzuri wa mitihani. Mkuu wa Wilaya, Chang’ah aliahidi kuunda tume ya uchunguzi kubaini sababu za tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment